MWL CHRISTOPHER MWAKASEGE: SOMO:HATUA ZA IMANI UNAPOSHIRIKI CHAKULA CHA BWANA ILI UPATE UPONYAJI NA AFYA KIROHO NA KIMWILI

 KONGAMANO LA 13 LA MAOMBI YA KITAIFA - DODOMA (UDOM) - 2021

NA MWL CHRISTOPHER MWAKASEGE
DAY-2,SESSION-1, 18 AUGUST, 2021
SOMO:HATUA ZA IMANI UNAPOSHIRIKI CHAKULA CHA BWANA ILI UPATE UPONYAJI NA AFYA KIROHO NA KIMWILI

Tangu Mungu alipotusemesha kuwa tuwe na cha chakula cha Bwana katika kongamano,Imekuwa si kitu chepesi sana kwangu maana lazima niende kwa Mungu kwa upya ili aseme kwa upya nasi tusishiriki kwa mazoea. Tangu tulipoanza kushiriki chakula cha Bwana katika Kongamano la maombi nina notes nyingi sana ambazo ningekuwa natumia uzoefu ningechagua mojawapo na ungepata kitu cha kukusaidia. Ila kwa Mungu hatuendi namna hiyo. Lazima twende barazani pa Bwana kuuliza kitu ambacho Mungu anataka kusema na watu wake. HATUA NNE MUHIMU HATUA YA KWANZA 1.SHIRIKI CHAKULA CHA BWANA KWA IMANI KWA JICHO LA UPONYAJI NA AFYA. Mathayo 15:21-21 Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile. Yesu alipokuwa anamjibu huyu mama juu ya kuomba uponyaji wa binti yake lakini Yesu alimwambia mambo ya chakula. Kwa hiyo alikuwa anahusianisha uponyaji na chakula. Alipokuwa anasema si vema kuwapa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Yesu alikuwa analinganisha chakula ambacho anacho na ombi la yule mama. Kwa hiyo Yesu alimjibu kile kitu ambacho alichoona na yule mama aliona uponyaji ndani ya Yesu. Yohana 6:51,55-57 Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Yesu hapa anasema yeye ni chakula. Yesu alimjibu yule mama aliona chakula ambacho Yesu anacho kutoka mbinguni kwa ajili ya uponyaji. Ndio maana hata yule mama aling'ang'ana na Yesu aliposema haifai kuchukua chakula cha watoto na kuwapa mbwa. Pia Yesu alimwambia kilicho fanya akaona kama alivyoona ni imani na ndio maana alisema mama imani yako ni kubwa. Katika Yohana 6 Yesu anajitambulisha kama chakula/mkate kutoka mbinguni ambao ndani yake kuna uzima Uzima=uhai +afya ya mwili na rohoni Unaweza ukawa na uhai na usiwe na afya ya Kiroho na Kimwili. Maana afya ni kwenye mwili na ndani ya roho. Yesu alipokuwa anashiriki Pasaka wanafunzi wake katika Luka 22:19 alipokuwa anamega mkate aliutambulisha kama mwili wake. Kama yule mama aliona kwa Yesu uponyaji hatutajua kama wanafunzi wa Yesu waliona kwa kiwango gani alipoutambulisha mkate kama mwili wake. Aliposema leo mnakula mwili wangu maana yake alikuwa anawaambia kuwa mnakula uponyaji na afya zetu. Hapa ni tungezumza kwa lugha ya yule mama. Katika Yohana 6:51 Yesu alisema mimi ndimi chakula chenye uzima kishukacho toka mbinguni mtu akila hiki ataishi milele. Pia utaona anazungumzia juu ya chakula akizungumzia mwili wake. Alisema mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Na mtu akishiriki hivyo ataishi milele. Ndani ya mwili wake kuna uwezo wa uponyaji ambao utatunza afya ya mwilini wako na roho yako.

Katika Luka 22:20. Anazungumzia Damu yake ya agano ni kinywaji ambacho anakitoa Mambo ya Walawi 17:1 Kwa kuwa uhai wa mwili uko katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. Uhai wa mwili upo katika Damu. Waliosomea mambo ya udaktari au bilologia wanajua damu imeumbwa kwa namna ya ajabu sana. Maana Damu ni uhai kwa maana hiyo ina maana roho inapita ndani ya damu na kuzunguka sehemu kubwa sana ya mwili. Damu ina chembechembe nyeupe za damu kazi yake ni kupamba na kitu chochote kigeni kinachoingia ndani ya mwili ili kisilete ugonjwa, na kuzuia na kupambana navyo ili visipate nafasi. Unaweza beba vidudu vya ugonjwa ndani ya mwili wako lakini haimaanishi kuwa wewe ni mgonjwa. Unachopojiona kuwa wewe ni mzima ni kwa sababu ya nguvu ya seli nyeupe za damu ambazo zinapambana. Huko ndiko imewekwa immunity system ambayo inamsaidia mwanadamu ili kudhibiti vitu vigeni vinavyoingia ndani ya mwili wake na kutunza afya yake. Na kama vile vidudu vimemletea ugonjwa basi vinapambana ili kuhakikisha kuwa vinadhibitiwa. Damu ya Yesu na yenyewe ina chembechembe ndani yake za uponyaji, uzima na afya. 1 Wakorintho 5:7 inasema Pasaka wetu amekwisha tolewa tayari yaani Kristo Bwana. Maandiko yanasema Kristo ni Pasaka kwetu. Neno Pasaka tunaliona katika Kutoka 12:11 hapa ndipo neno pasaka lilipoibukia. Baada ya Musa kuwaeleza wana Israeli juu ya pigo la mwisho kabla ya kutoka Misri. Baada ya kuwapa maelezo namna ya kumchinja kondoo. Katika ile mstari wa 11 anatoa maelezo namna ya kumla na baada ya maelezo anasema huyu ni Pasaka wa Bwana. Yule mama mkananayo ambaye mwanae alikuwa na mapepo alienda kwa Yesu maana alijua kuwa ni chakula cha uzima. Katika damu ya ile kondoo ilicho fanya ni kuwafungua wana Israel katika kifungo cha Farao. Unaweza ukawa umefungwa na usijue kuwa umefungwa. Yusufu alikuwa waziri mkuu lakini bado ni mtumwa maana hakuwa kwao. Yusufu alipokuwa jela alipewa cheo lakini bado akikuwa mfungwa. Hata vipawa vya Roho Mtakatifu vilikuwa vinafanya kazi lakini bado alikuwa jela. Damu ile iliwafungua kutoka katika vifungo vya Farao lakini pia ilihakikisha kuwa wanatoka maana unaweza kutangaziwa kutoka na usitoke jela.Damu ilihakikisha wakiwa safarini wawe na afya. Miguu yao haikuvimba. Yesu Kristo ni Pasaka wetu, kwa hiyo ile damu ya Yesu inafanya kwa ubora zaidi kuliko ile damu ya Kondoo iliyowatoa wana Israel Misri. Ndani yake imebeba nguvu ya kukufungua utoke kwenye ugonjwa na kukusaidia uweze kuishi kwenye afya baada ya kupona ugonjwa. Unaweza ukapona ugonjwa wako na afya yako isirudi vizuri. Shiriki chakula cha Bwana kwa jicho la uponyaji na afya. Yule mama alikuwa anaona uponyaji na afya ukitembea na Yesu. Ndio maana Yesu alimwambia imani yako ni kubwa. Nilipokuwa namuomba Mungu kuwa umeweka nini ndani yake chakula cha Bwana mwaka huu alisema. Nimeweka Uponyaji na afya Hasara ya dhambi ni kumuondolea mwanadamu kinga ya afya ya kiroho. Basi uwe na uhakika utatafuta uponyaji wa mwili wako na roho yako. Yesu pale msalabani alichukua magonjwa yetu na udhaifu yetu. Kuna watu wanaokoka na kupata uponyaji saa hiyo hiyo. Kuna tofauti ya uponyaji na afya. Uponyaji ni kutoa ugonjwa ulioingia ndani yako au kuuzua usipate. Afya ni mfumo wa maisha. Haitoshi tu kula chakula cha afya lazima uishi maisha ya afya. Fikra zako lazima ziwe sawa. Ndio maana madaktari wanajua kabisa kuna aina fulani ya kuwaza kunakausha mifupa. Afya inategemea na mazingira ambayo unaishi. Unaweza ukapona Malaria lakini kama unakaa katika mazingira ambayo ya mtu ujue tu utaugua Malaria. HATUA YA PILI. 2.SHIRIKI CHAKULA CHA BWANA KWA IMANI KIAGANO JIPYA KAMA CHAKULA KUTOKA MBINGUNI. Yohana 6:51 Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Luka 22:19-20. Siku Yesu alipokuwa anashiriki chakula cha Bwana na wanafunzi wake.
Wanafunzi wake walimuandalia pasaka ya agano la kale ila yeye aliifanya kiagano jipya. Yohana 6: 48,50-51 Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa.Mimi ndimi chakula cha uzima. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Yesu alisema mimi nimebeba chakula ambacho ni bora na ni zaidi kuliko mana.Na anasema kama mtu akila chakula hiki ataishi milele. Kama mana iliwatunza miaka 40 bila kuugua isipokuwa walipomkorofisha Mungu. Miguu yao pia haikuvimba walikuwa na afya nzuri. Mathayo 15:21-28 26 Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Uponyaji ni chakula cha watoto na ndio halali yao. Yesu alisema sio halali kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Ilikuwa ni lugha ya imani ndio maana yule mama hakukasirika. Yule mama alisema hata kama huwezi kunipa chakula basi naomba hata makombo. Yule mama alijua kuwa chakula ambacho Yesu anatoa kinabaki. Na ndio maana aliona thamani ya chakula ni kubwa sana.Yule mama aliona uponyaji kwenye mkate ukiwa mezani au chini (makombo). Muujiza wa Yesu katika ile mikate mitano na kulisha watu 5000. Wakala na wakasaza. Je umewahi kujiuliza kwanini Yesu alisema okota vipande vya mkate na si vipande vya samaki Yesu ni mkate ushukao, alisema hamuwezi kumaliza kitu ambacho nawapa. Ndio maana baada ya ule muujiza walipata vikapu 12 vya mikate. Maana yake kila Mwanafunzi kikapu kimoja kimoja. Thamani ya mkate ni sawa na makombo ya mkate. Kilichobadilisha thamani ya mkate ukiwa chini na ulio chini tofauti ni meza ambayo inawekwa ni imani. Ila mkate ni mkate ukiwa juu ya meza au chini ya meza. Yesu aliposema chakula hiki ni cha watoto maana yake alikuwa anazungumzia uhalali wa kukila kwa namna ya agano. Kula kwa kadri unavyosikia. Inategemea ndani yake unakula kwa namna gani. Wengine wanashiriki mara moja kwa mwaka, au kwa mwezi wengine kila jumapili na wengine kila siku na wengine hawashiriki kabisa. Biblia inatuambia wazi kabisa kuwa Chakula cha Bwana kilianzia nyumbani kwa hiyo kushiriki nyumbani ni sawa kabisa cha muhimu ni imani yako. Haijalishi umejificha mahali pagumu kiasi gani Yesu anakuona. Maana Yesu ni chakula kishukacho kutoka mbinguni. Kwa hiyo kikishuka hakikisha unakula. HATUA YA TATU 3 TUMIA KUSEMA IMANI YAKO ILI KUBADILI CHAKULA CHA BWANA KILICHOWEKWA MBELE YAKO KIWE UPONYAJI KA AFYA. Mathayo 15:28 Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile. Yesu aliona imani ya yule mama katika maneno.Kwa imani yake yule mama aliona chakula na uponyaji katika makombo wakati wengine hawajaona. Kwa hiyo alielewa lugha ya Yesu. Kwa hiyo hakukubali lugha ya Yesu imkwamishe. Kwa hiyo alisema mimi kama sio halali kama mtoto wako kula chakula hicho basi naomba ikiwa chakula kitadondoka katika meza yako naomba usikitupe mimi nitakula. Kwa hiyo alikuwa anasema juu ya imani yake. Yesu alipokuwa anasema juu ya chakula Yule mama aliona uponyaji katika chakula. Yesu alipobadili uponyaji kuwa chakula. Yule mama aligeuza chakula cha Yesu kuwa uponyaji. Yesu alimwambia imani yako ni kubwa na iwe kwako kama utakavyo. Watoto wa Mungu wakila chakula katika meza ya Bwana kama chakula cha kawaida hawapati kitu.Maana kinakuwa tu kama chakula cha kawaida. Na watoto wengine ambao si halali kwa kuzaliwa mara ya pili kama watoto wa Mungu wakila chakula kile kile kwa imani wanapata uponyaji. Kinachobadili chakula kuwa uponyaji sio meza iliyopambwa vizuri. Meza haibadilishi aina ya chakula.Kama makombo yanaweza mponya mtu maana yake uponyaji uliopo kwenye chakula cha Bwana hautegemei meza. Kwa hiyo andaa meza kwa imani na shiriki pia kwa imani. Eliya alipokuwa amechoka aliomba Mungu atoe roho yake alilala akisubiri akiamka awe upande wa pili. Malaika kutoka mbinguni akaja akamwambia amka ule. Akaamka akala na akalala.
Malaika akamwamsha mara ya pili na akaambiwa amka ule maana una safari mbele. Akaamka akala na akasonga mbele kwa siku 40. Lile neno lilimsaidia kujenga imani yake. Kwa hiyo usiwashirikishe watu chakula cha Bwana kwa mazoea. Lazima kuwe na neno ambalo linawapa imani.Yesu ni chakula kilichoshuka kutoka mbingu. Shiriki chakula kwa neno ili ijenge imani ndani yako. Kutoka 12:1-11. Biblia inazungumzia juu ya Amri ya Mungu, ya kwamba kila familia moja itafute kondoo na imuweke kwenye zizi kwa siku 14. Biblia inasema wakati wa jioni atatolewa na kuchinjwa na imetoa na maelekezo ya namna ya kumchinja. Kitu kilichobadilisha kondoo wa nyama choma kuwa kondoo pasaka ni neno la imani ambalo Mungu alilitoa kwa Musa na Musa alikifikisha kwa Wana Israel. Tumia neno la Bwana kubadilisha chakula kuwa Pasaka kwa imani. Kwa hiyo sema maana imani inaonekana katika maneno. Sakramenti ambayo Yesu alishiriki ilikuwa ni ni sehemu ya kawaida. Kitu kilichobadilisha mkate kuwa mwili wa Yesu ni neno ambalo Yesu alilosema. Hata baada ya kuchukua kinywaji alisema damu yake inayomwagika kwa ajili ya ondoleo oa dhambi. Kilichobadilisha mkate kuwa mwili ni kusema( yaani kusema kwa imani). 2 Wakorintho 4:13 Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani; kama ilivyoandikwa, Naliamini, na kwa sababu hiyo nalinena; sisi nasi twaamini, na kwa sababu hiyo twanena Kama una aamini ndipo unasema unacho amini maana yake unasema imani yako. Kwa hiyo umeweka imani yako katika maneno yale yaliyoingia ndani yako. Maana imani huja kwa kusikia. Kwa hiyo unapokisema inakuwa ni binafsi kwako yaani unasema kile ambacho una uhakika nacho. Maana imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo. Na utaenda kupokea sawa sawa na imani yako. Unanena kwa sababu kuna kitu unachoamini. Huwezi kushiriki kwa imani kama huna neno ambalo linajenga imani ndani yetu. Maana yule mama mkananayo ina maana kuna mahali alisikia kuwa Yesu ni chakula kishukacho kutoka mbinguni. Hata Yesu hata alipo amua kusema kama alivyosema lakini bado yule mama aliona imani yake. Maana imani huja kwa kusikia. Hata wewe jifunze kusema kile ambacho unaamini juu ya chakula cha Bwana na utapata kile ambacho unasema. HATUA YA NNE 4.TUMIA IMANI KUGEUZA KITENDO CHA KUSHIRIKI CHAKULA CHA BWANA KIWE HATUA YA KUPOKEA ULICHOAMINI KIMO KWENYE CHAKULA CHA BWANA. Hatua ya tatu inabadilisha chakula cha Bwana kiwe uponyaji. Ndani ya chakula cha Bwana kuna vitu vingi sana. Uponyaji na afya ni kitu kimojawapo tu. Waebrania 11:28 kwa imani akaifanya Pasaka. Kwa hiyo kilichobadilisha kondoo kuwa Pasaka ni imani ambayo Musa aliisikia kutoka kwa Mungu. Alisema alichoamini akapata alichosema kwamba kitatokea wakishiriki. Hii inabadilisha kitendo cha kile ambacho unakitumia kushiriki kiwe kitendo cha kwenda kupokea.Maana yake kile ambacho kimo ndani ya chakula cha Bwana unaamini unakwenda kupokea. Soma: Waebrania 11:1. Warumi 10:17 , Yakobo 2:17,20 mistari hii yote inazungumzia imani. Ile kwamba una Imani lazima inaonekana kwenye kitendo maana ndipo unaenda kupokea. Mfano wa mama aliyetokwa na Damu miaka 12 alisema moyoni mwake nikigusa pindo lake nitapona. Angeweza kusema kuanzia asubuhi mpaka jioni na asingepona. Lakini alipochukua hatua ya imani ya kutoka nje ili akaguse pindo la Yesu kupona. Alipokuwa anatafuta pindo la Yesu hakuwa anatafuta maombi bali alikuwa anatafuta mahali pa kuunganishia imani yake ili apokee uponyaji. Watu wengi waliokuwa wanakwenda kwa Yesu walikuwa wanakwenda kuponywa na sio kuombewa. Mara nyingi Yesu alikuwa anawaambia imani yako imekuponya au imekuokoka. Wengi sana waliponywa kwa imani zao na ni wachache sana waliponywa kwa imani ya Yesu. Imani ikiwa moyoni inakuwa mdomoni na kuwa kwenye matendo.Shiriki ukiwa na imani ya kupokea. Unapokea kitu ambacho unaenda kuchukua.Kitendo cha imani hakitakiwi kitendo cha kawaida. Soma Mathayo 9:27-31 Yesu alikuwa anasema kwa kadri ya imani yenu mpate. Angalia na 1 Wakorintho 11:24- 26 Katika Mathayo 9:27-31 Yesu aliwauliza swali la imani. Ndani ya yale maneno. Yesu alisema kwa kadri ya imani yako upate. Msalaba ulitoa kila kitu kwa 100%.

Kinacho tofautisha ni imani ndio inaamua upate kiasi gani. Imani yako ikiwa kubwa ndipo inaamua kiasi gani upate. Yesu anataka ushiriki chakula cha Bwana ili usisahau kitu iwe kumbukumbu… Ushuhuda. Wakati fulani alikuja mtu mmoja kushiriki hapa kwenye kongamano ambaye sio Mkristo. Kile kitu ambacho alipata siku ile alikuja tena kesho yake kuja kushiriki tena lakini siku hiyo alipokuja tena tulikuwa hatushiriki. Kumbuka huyu mama hakuwa Mkristo lakini alipata kitu katika kushiriki chakula cha Bwana. Wale Vijana wa Emausi walipokuwa na Yesu alipowapa kile chakula tunaona walifumbuliwa macho yao na wakati huo huo Yesu akatoweka kati yao. Wana Israel walipewa kile chakula kiliwasustain maisha yao. Ndio maana Mungu aliwapa kile chakula. HATUA YA TANO. KILE UNACHOPATA KATIKA CHAKULA CHA BWANA SHETANI ANAKUJA KUPINGANA NACHO Maana yake uwe na imani ya kupigania kile ulichopokea. Imani inaendelea kukushukilia. Kwa hiyo usiwe na imani tu ya kupokea bali uwe na imani ya kushikilia kile ambacho Mungu kakupa. Maana baada ya kushiriki shetani atataka kukuonesha kama hujapona au vyoyote ila wewe shikilia kile kitu ambacho Mungu kafanya kwako. Hata wewe unayesoma somo hili unaweza andaa chakula cha Bwana. Kama tulivyojifunza hapa na weka imani yako katika kitu ambacho unafanya na utapokea kitu kutoka kwa Bwana. Pia kama Roho Mtakitatifu atakusukuma kuambatanisha sana sadaka basi tumia namba zetu za sadaka katika link iliyopo pale juu. Ubarikiwe sana 🙏🙏🙏🙏

Maoni