MWL CHRISTOPHER MWAKASEGE SOMO: NGUVU YA KUOMBA TOBA TOKA KATIKA NAFASI YA KUHANI

  KONGAMANO LA 13 LA MAOMBI YA KITAIFA - DODOMA (UDOM) - 2021 NA MWL CHRISTOPHER MWAKASEGE

DAY 1, SESSION 2 TAREHE 17 AGOSTI, 2021
AGENDA: KUOMBA KWA AJILI YA TATIZO LA UGONJWA WA CORONA
SOMO: NGUVU YA KUOMBA TOBA TOKA KATIKA NAFASI YA KUHANI


Ufunuo 5:9-10 Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi. Kazi mojawapo ya Damu ya Yesu iliyomwagika pale msalabani baada ya kutuzaa mara ya pili, tunapewa nafasi mbalimbali mojawapo ni ukuhani. Kila mtu aliyeokoka ni kuhani. Kuna watu wanalitazama hili jambo kwa jicho la agano la kale la kuona baadhi ya watu ndio makuhani yaani kama wachungaji au watumishi fulani fulani hivi. Ukiingia ndani ya Yesu kuna nafasi unapewa kwa hiyo ni suala la wewe kuamua kuitumia au kutoitumia.  Ukisoma habari za mwanampotevu alipoenda nchi ya mbali na kutapanya mali yite. Alipozingatia moyoni mwake aliamua kurudi nyumbani kwa baba yake. Yeye alijipangia kuwa awe mfanyakazi ila baba yake alimrudishia nafasi yake ya kuwa mtoto. Hili tunajifunza pia kuwa Mungu hurudisha nafasi yako uliyoipoteza baada ya kutubu hata kama ulikosea namna gani maadamu ukitubu, Mungu atakusamehe na kukurudishia nafasi yako. Kwa hiyo ni suala lako la kuamua kuichukua au kuikataa. Waebrania 9:7 Lakini katika hema hiyo ya pili kuhani mkuu huingia peke yake, mara moja kila mwaka; wala si pasipo damu, atoayo kwa ajili ya nafsi yake na kwa dhambi za kutokujua za hao watu. Kazi mojawapo ya kuhani ni kufanya toba kwa ajili ya watu. Na usisubiri mpaka watu wameacha dhambi ndipo uombe toba kwa ajili yao. Huhitaji kibali chao ili kuwaombea toba. Kuhani ana uwezo wa kuomba toba kwa watu hata wakitenda dhambi kwa kutokujua kuwa wamefanya dhambi. Pia anaweza kuomba toba kwa ajili ya watu ambao wametenda dhambi kwa kujua. Kuhani ili aweze kukubalika anahitaji kuingia madhabahuni kwa Bwana kwa Damu ya Yesu. Sisi kama makuhani tunapaingia patakatifu kwa Damu ya Yesu. Mathayo 26:28 Kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Waebrania 9:22 Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. Hapa hazungumzii Damu ya Yesu kufanya kazi ya kusamehe bali hapa anazungumzia Damu ya Yesu kuondoa. Kuna tofauti ya kusamehewa dhambi na kuondolewa dhambi. Katika agano la kale walikuwa wanaweza kusahemewa dhambi na sio kuondolewa dhambi. Katika agano la kale palikuwa na kumbukumbu la dhambi mwaka kwa mwaka. Mungu hawezi kuondoa dhambi bila kusamehe kwanza, akisamehe ndipo anaondoa dhambi. Waebrania 9:19-22 Maana kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyoamuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote, akisema, Hii ni damu ya agano mliloamriwa na Mungu. Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada alivinyunyizia damu vivyo hivyo. Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. Tafuta Biblia ya (Amplified Bible) halafu soma hii mistari. Damu ya Yesu haishughulikii tu na kuondoa dhambi bali inaondoa chanzo cha dhambi, dhambi yenyewe na madhara ya dhambi. Biblia inasema aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi. Hii sio sababu ya kuwa hawatendi dhambi bali ni kwa sababu ile mbegu ya dhambi imeng'olewa. Katika agano la kale hiki kitu hakikuwepo na ndio maana katika agano jipya Damu ya Yesu ilikuja ili iweze kutatua shida ya dhambi. Damu ya Yesu ikiachiliwa mahali inaweza kufanya vitu vyote vitatu kwa wakati mmoja yaani kusamehe, kuondoa dhambi na kuondoa madhara ya dhambi. Suala la Mungu kukusamehe hajadiliani na mtu, kuwa nikusaheme au nisikusamehe? Yeye anakusamehe kama apendavyo.

Ukienda kwa Mungu kwa imani Mungu anakusamehe na kukuondolea dhambi. Maana yake unahesabiwa haki na Mungu. Waebrania 8:6 Lakini sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora. Hapa inazungumza habari za Yesu za kuwa kuhani mkuu. Waebrania 8:1. Kwa hiyo kuwa kuhani mkuu ina maana kuna makuhani chini yake. Ile kwamba kuna mkurugenzi mkuu ina maana kuna wakurugenzi chini yake na wanafanya kazi pamoja ila sasa kuna mkuu wao yaani mkurugenzi mkuu. Kama Yesu amepewa huduma iliyo bora zaidi ina maana na sisi tumepewa huduma iliyo bora zaidi. Sisi ni wajumbe wa agano lililo bora. Kwa hiyo tuna huduma iliyobora kuliko ile ya Haruni. Hii ni kwa sababu katika agano la kale Haruni alipewa ukuhani kwa mfumo huo. Ila katika agano jipya tunachukua heshima ya ukuhani kutoka kwa Yesu kwa mfano wa Melkizedeki. (Biblia ya kiswahili inasema “kwa mfano” ila ya kiingereza inasema "order of Melchizedek"). Ukienda katika ngazi ya kisiasa kwa mfano utaona ya kuwa kuna nchi nyingi sana Duniani zina viongozi ambao wanaitwa Marais. Na nguvu zao zinatofautiana kutokana na katiba ambayo wamepewa. Kuna nchi zingine Rais ana nguvu sana, lakini zingine waziri mkuu ana nguvu kuliko Rais. Yesu kama kuhani mkuu nguvu aliyopata ilitokana na agano jipya ambalo alilipata kwa Damu yake kumwagika Msalabani na Mungu kumpa hiyo nafasi. Agano la kale lilikuwa na nguvu wakati ule ambapo Mungu aliwapa. Ila sasa agano jipya lina nguvu zaidi kwa sababu ya Damu ya Yesu ambayo ilimwagika msalabani na ndilo agano lililo bora zaidi. Ukuhani wetu umejengwa juu ya ukuhani wa kutoka kwa Yesu katika Damu yake. Na sio kutoka kwa Haruni. Hakuna kuhani anaruhusiwa kuingia patakatifu pa patakatifu bila Damu ya Yesu. Heshima tunayopata ni kwa sababu ya aina ya Damu ambayo Mungu katupa. Kwa hiyo tukiomba toba kwa Mungu wetu na Mungu akikubali toba yetu, toba hiyo inakuwa na  nguvu zaidi kwa sababu ya Damu ya Yesu ambayo tunaitumia. Ni Damu bora sana katika ulimwengu wa roho. Hesabu 16:41-50 Lakini siku ya pili yake mkutano wote wa wana wa Israeli wakamnung’unikia Musa, na Haruni, wakasema, Ninyi mmewaua watu wa BWANA. Basi ilikuwa, hapo huo mkutano ulipokuwa umekutanika kinyume cha Musa, na kinyume cha Haruni, wakaangalia upande wa hema ya kukutania; na tazama, hilo wingu likaifunika hema, na utukufu wa BWANA ukaonekana. Na Musa na Haruni wakaenda hapo mbele ya hema ya kukutania. Ondokeni kati ya mkutano, ili niwaangamize mara moja. Wao wakapomoka kifudifudi. Musa akamwambia Haruni, Haya, shika chetezo chako, ukatie moto ndani yake, moto wa madhabahuni, kisha utie na uvumba juu ya moto, ukakichukue haraka, wende nacho katika huo mkutano, ukawafanyie upatanisho; kwa kuwa ghadhabu zimetoka kwa BWANA; hiyo tauni imeanza. Basi Haruni akakishika chetezo kama Musa alivyonena, akapiga mbio akaenda katikati ya mkutano; na tazama, tauni ilikuwa imeanza kati ya watu; akatia uvumba juu ya moto na kufanya upatanisho kwa ajili ya hao watu. Akasimama kati ya hao waliokufa na hao waliokuwa wakali hai; tauni ikazuiwa. Basi waliokufa kwa tauni walikuwa kumi na nne elfu na mia saba, zaidi ya hao waliokufa katika jambo la Kora. Haruni akamrudia Musa pale mlangoni pa hema ya kukutania; hiyo tauni ikazuiwa. Tauni maana yake ni ugonjwa wa kuambukiza ambao hata madaktari hawajui chanzo chake. Kitu ambacho wanafanya wanaweka lockdown. Kwa hiyo ikitokea tauni katika eneo fulani kwa ajili ya nguruwe wanazuia nguruwe kuingia au kutoka katika eneo hilo. Lengo lake ni kuzuia tauni isienee. Tauni ni adhabu, tunaweza kuwa na kila maelezo ya kueleza chanzo chake kitalaamu ila kikubwa ni adhabu katika ulimwengu wa roho ambayo Mungu anaiachilia. Madaktari wanaweza kuwa na utalaamu wao na sisi kama waombaji tuna utalaamu wetu katika ulimwengu wa roho katika kutibu hilo. Na wote tutakuwa tunafanya kazi ya Bwana. Wakati ule  wa Haruni ambapo walikufa watu 14,700 kama wangekuwepo madaktari wangesemaje? (Yaani wangekuwa na sababu zao za kitalaamu za kuuelezea ugonjwa huu)

Sasa tupo katika Msimu mpya ambao umefunguliwa katika  lango  ambalo lilifunguliwa na ugonjwa wa Corona.  Sasa tukirudi kwenye somo letu kuwa wale watu waliokufa katika kitabu  Hesabu 16:41-50 ni kwa sababu Haruni alichelewa kufika maana yake alipofanya toba  na ile tauni ikazuiliwa. Ile Damu aliyobeba ndio iliyochora  mstari. na kufanya tauni kuzuiliwa. Kazi mojawapo ya Damu ya Yesu ni ondoleo. Yaani kuondoa dhambi na chanzo chake pamoja na madhara yake. Dawa ya Ugonjwa wa Corona ni toba. Kama Haruni maombi yake yalisikiwa  kwa sababu ya kuwa kuhani je si zaidi sana maombi katika wakati huu wa agano jipya ( agano lililo bora zaidi?)  Kama Mungu aliheshimu maombi ya Haruni basi Mungu ataheshimu maombi yetu katika Kristo. Kama alijibu ya Haruni basi na ya kwetu atajibu pia. Kwa nini sisi tunaona kama vile tukifanya toba Mungu hajibu kama alivyofanya wakati ule wa Haruni. Sababu mojawapo ni kutokuamini kwetu. Chukua kwa mfano watu 14,700 walienda mbinguni na wakachungulia  huku Duniani na kuona kuwa kuna watu wamepona. Haruni akienda mbinguni. Wanaweza muuliza sana maswali. Kwa nini ulichelewa kuja kuomba toba na umeacha tumekufa? Ona sasa nimeacha watoto yatima na hata mambo yangu ya benki sikuweka sawa. Ona sasa nimewaachia watoto madeni. Kwa hiyo nataka tukaombe hapa na tuombe kwa nafasi ya kikuhani. Kwa kuomba toba kwa ajili ya Ugonjwa wa  Corona. Kama nyumbani kwako una watoto utajua kabisa kuwa wana nafasi tofauti tofauti ndani yako. Kuna mmoja akiomba jambo hata hujiulizi ila mwingine akiomba lazima utasema ngoja kidogo. Ni vivyo hivyo hata sisi tukiomba toba kutoka katika nafasi ya kikuhani Mungu anatusikia. Wakati fulani tulikuwa Tanga. Mungu alinionyesha mambo kadhaa kwa watoto na watu walioko kanisani na wasichana. Nikaomba Mungu kwa kusema, Mungu nakuja mbele zako kama Kuhani naomba toba kwa ajili ya mambo ambayo umenionyesha. Nikiomba namna hiyo katika ulimwengu wa roho nabadilisha gia (gear). Neema inatoa, imani inapokea. Ukikaa kwenye nafasi yako hamna mtu anaweza kukunyang'anya.  Mungu katupa nafasi ya kikuhani  na tuipokee kwa imani kwa hiyo tuombe toba  kwa kutumia nafasi hii kwa ajili ya nchi  ili Mungu atuondolee huu ugonjwa wa Corona (COVID-19). Omba maombi ya toba kwa ajili ya nchi dhidi ya ugonjwa wa Corona. Unapoomba kwa ajili ya Tanzania ombea na nchi zingine ili Mungu aponye Dunia yote na kuondoa madhara ya ugonjwa wa Corona (COVID-19).


Maoni