MWL CHRISTOPHER MWAKASEGESOMO: UPONYAJI WA TAIFA KUPITIA CHAKULA CHA BWANA

 KONGAMANO LA 13 LA MAOMBI YA KITAIFA - DODOMA (UDOM) - 2021

NA MWL CHRISTOPHER MWAKASEGE
DAY-1,SESSION-2 TAREHE 19 AUGUST, 2021

SOMO: UPONYAJI WA TAIFA KUPITIA CHAKULA CHA BWANA
Bwana Yesu asifiwe sana. Katika kongamano hili tuna uwakilishi wa nchi kadhaa:- Marekani, Canada, Sweden, Kenya, Scotland, Congo DRC, Qatar, Burundi, Rwanda, Zambia, na wenyeji Tanzania. Katika kujifunza somo hili nataka ujiulize swali hili la kuwa kama Mungu anakusemesha kushiriki chakula cha Bwana muulize kuwa katika chakula hicho kaweka nini. Hii itakusaidia kunyanyua imani yako. Kwa hiyo kila mtu atashiriki kwa niaba ya Taifa lake.
Luka 22:19 Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.] Yesu anasema katika mstari wa 15 kuwa alikuwa na kiu ya kuila Pasaka pamoja nao. Kwa hiyo Yesu huenda huko nyuma alitamani siku moja aweze kushiriki Pasaka na wanafunzi wake ila katika mazingira ambayo alikuwa nayo kila mwanafunzi ikifika wakati huo wa Pasaka alikuwa anaenda kwenye familia yake. Huu ndio ulikuwa utaratibu wa Wayahudi mpaka leo. Wakati huu alitamani ashiriki pamoja na wanafunzi wake na ndio maana alisema nina kiu kubwa. Kwa hesabu ya wanafunzi walikuwa 12 na Yesu alikuwa ni wa 13. Wakati Yesu anampa mkate Petro alikuwa anaona nini? Pia je wakati anampa Mathayo alikuwa anaona nini?. Ukitazama kwa haraka pale unaweza kuona alikuwa anawapa tu wale wanafunzi wake 12 kama waanzilishi wa kanisa. Angalia Yohana 17:20 :- Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. **Mathayo 28**18-20 Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari. Yesu alipokuwa anafanya maombi kwa ajili ya wanafunzi wake alikuwa haoni wanafunzi tu pale bali na watu ambao wataliamini neno ambalo wanafunzi watasema. Kwa hiyo Yesu aliombea na matokeo ya watu ambao wanaamini neno kupitia neno ambalo wanafunzi watasema. Wakati Yesu anawapa mkate wanafunzi wake alikuwa anaona na watu wengine ndani yao. Ukiangalia katika Mathayo 28, Yesu anazungumzia juu ya mamlaka yote mbinguni na duniani. Sasa kwa nini awape mamlaka mbinguni na duniani wakati hawa jamaa huduma yao itaishia Israel tu. Ukimtazama Paulo kwa mfano yeye alienda na maeneo mengine na baadhi ya wanafunzi walienda mbali kidogo na nchi yao ya Israel kupeleka injili. Lakini swali najiuliza kwa nini awaeleze mamlaka aliyonayo kwa ajili ya Tanzania kama hawatafika huku Tanzania? Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,.... Na Biblia inazungumzia kuanzia Yerusalemu. Sasa kama unasoma Biblia ya kiingereza lile neno Mataifa yote lina tafsiri kadhaa ndani yake. Tafsiri ya kwanza ni ndani ya watu walipo ndani ya mataifa tofauti tofauti. Pia tafsiri nyingine inazungumzia taifa kama taifa. Yaani to disciple nations. Wakati anawatuma wanafunzi wake kuhubiri injili, Yesu alijua kabisa Petro hatafika Tanzania lakini alisemea enendeni. Hilo halikuwa agizo kwa ajili yao peke yao bali kwa ajili ya kila mmoja ambaye ataliamini neno kwa ajili ya kile kitu ambacho watakuwa wanasema kwa ajili ya Yesu. Assignment ya kitu walichopewa iliwekwa ndani ya kila mmoja kwa ajili ya kitu ambacho wamepewa ili wengine waje kumuamini Yesu. Yesu alifunga agano jipya na watu 12. Maandiko yanasema atafunga agano jipya na kabila la Yuda na Israel. Maandiko yanasema pia kuwa Kanisa ni sehemu ya agano jipya. Sisi tunafaidi matunda ya agano jipya kwa Mungu wa Israel kwa sababu Yesu aliachilia agano jipya.

Maoni